8 Aprili 2019 - 09:24
Wasudani waandamana kumpinga rais

Maelfu ya waandamanaji nchini Sudan jana Jumapili walifanya maandamano nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Maelfu ya waandamanaji nchini Sudan jana Jumapili walifanya maandamano nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum kwa siku ya pili, wakilitaka jeshi kuunga mkono madai yao ya kumtaka Rais Omar al Bashir ajiuzulu. Eneo hilo pia ndilo makao makuu ya Wizara ya Ulinzi na makaazi rais ya Rais, ambaye waandamanaji wanataka kuumaliza utawala wake wa karibu miaka 30. Waandamanaji walisikika wakitamka maneno ya "Sudan inainuka, jeshi linainuka". Waandamanaji waliwarushia mawe polisi ambao walitumia mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na virungu katika kujaribu kuwatawanya waandamanaji hao. Wawakilishi wa upinzani pamoja na duru moja ya matibabu wamesema jana kuwa vikosi vya usalama viliwauwa waandamanaji watano katika maandamano hayo ya siku mbili. Aidha nchi hiyo ilitumbukia gizani baada ya kupotea nguvu za umeme. Haikufahamika maramoja kama ukosefu wa umeme ulihusishwa na maandamano hayo. Huduma za umeme zilirejeshwa katika baadhi ya maeneo ya nchi jana jioni.

Mwisho wa habari / 291